Friday, April 13, 2012

MCHAWI KUTOKA MBINGUNI


Siku moja Masudi alidamka saa 8 usiku kwenda msikitini kwa ajili ya kuwahi sala ya asubuhi yaani saa kumi na moja kwa vile inabidi atembee umbali mrefu mpaka afike msikitini. Basi akiwa njiani akakutana na kundi la watu ambao hawakua kwenye hali ya kawaida, akapatwa na hofu kubwa lakini akapiga moyo konde akaendelea na safari yake, baada ya mwendo kidogo akakutana na kundi lingine la watu wasio wa kawaida wakiwa uchi wa mnyama na wanaimba katika lugha ambayo ni tata wakija uelekeo wake, akapatwa na hofu kubwa ikabidi akimbie mbie mpaka sehemu akakuta kuna mbuyu mkubwa akapanda juu yake ili ajifiche wasimuone, kumbe na wale watu walikua ni wachawi na walikua wanaelekea kwenye mbuyu huo huo kwa ajili ya kikao chao cha asubuhi, basi Masudi alikuwa anawatazama na kuwasikiliza huku akitetemeka na kutokwa na jasho jingi.


Basi wale wachawi walianza kikao chao kwa kujitambulisha kama ifuatavyo
MCHAWI 1: Mimi naitwa joe ni mchawi kutoka Marekani.
MCHAWI 2: Mimi naitwa Madebe ni mchawi kutoka Afrika ya kusini.
MCHAWI 3: Mimi naitwa Juan ni mchawi kutoka Marekani ya kusini.
MCHAWI 4: Mimi naitwa Tony ni mchawi kutoka Ulaya.
Masudi akashangaa kidogo "enhee"
MCHAWI 5: Mimi naitwa Onyango ni mchawi kutoka Afrika mashariki.
MCHAWI 6: Mimi naitwa Cho ni mchawi kutoka China.
MCHAWI 7: Mimi ni Sheikh Baraghash natoka Falme za Kiarabu.

Masudi akashangaa mpaka akateleza kutoka kwenye mti akadondokea katikati ya uwanja, akitua chini kwa makalio yake. Basi wale wachawi wakashtuka kidogo, kwa mshangao yule mwenyekiti wa kile kikao cha wachawi akamuuliza Masudi "enhheeeee, hebu tuambie na wewe umetoka wapi?" Masudi akajibu haraka huku akitetemeka "Mimi ni Mchawi kutoka Mbinguni."