Friday, April 13, 2012

VITUKO NDANI YA DALADALA


Kweli dunia hii kila kukicha vituko haviishi, hii ilitokea hivi karibuni katika daladala moja litokalo Temeke Mikoroshini kwenda Mwenge jijini Dar.
Nikiwa nimekaa kwenye siti na mzee mmoja aliyeonekana kuwa ni mstaarabu kwa mavazi na umbile lake lililokaa kiafisa, nilishangaa kumuona akitoa hirizi badala ya fedha mfukoni mwake.
Mzee huyo licha ya kushika magazeti ya siku ile yakiwemo ya kimombo, alikuwa na kitabu kikubwa cha kuandika kumbukumbu na mambo yake muhimu maarufu kama Diary.



Ilionesha wazi kuwa alikuwa akienda au kutoka kazini, kwa jinsi alivyokuwa mstaarabu alipokaa kwenye siti alinisabahi.
Daladala lilipokuwa likiendelea na safari mzee yule alikuwa ‘bize’ akiperuzi habari zilizoandikwa kwenye magazeti.
Gari likiwa limeshika kasi, kondakta alianza kuchukuwa nauli kwa abiria kwa mtindo wa kuliza sarafu alizokuwa amezishika mkononi.
Yule mzee kila alipogongewa fedha na kondakta, hakusikia kwani alikuwa amezama kwenye mojawapo ya gazeti, ilibidi nimshtue, mzee yule bila kuhamisha macho yake kwenye gazeti aliachia mkono mmoja na kuuingiza ndani ya koti na kutoa noti ambayo ilikuwa imeambatana na hirizi nyeusi iliyodondoka bila mwenyewe kujua.
Kibaya zaidi wakati ananyoosha mkono, hakuangalia zaidi ya kuwa bize kusoma gazeti bila kujua kama alidondosha hirizi pembeni yangu.
Sikutaka kumshtua haraka niliacha kwanza kondakta amalize kukusanya fedha ndipo nilipomwambia;
”Samahani mzee.”
“Bila samahani, aliacha kusoma na kunitazama.
Nilimuonesha hirizi yake kwa ishara ili nisimuumbue, mzee baada ya kuiona alishtuka sana. Aliichukua haraka na kuirudisha mfukoni na kunishukuru kwa sauti ya chini.
“Ooh! Asante sana kijana.”
Nilimkubalia kwa kunyanyua kichwa, nilishangaa kumuona ameacha kabisa kusoma magazeti.
Licha ya kumwambia kondakta angeteremkia Mwenge, aliteremkia kituo kilichofuata ndipo nilibaini alifanya hivyo sababu ya aibu.
Baada ya kuteremka nilibaki nikiwaza kuhusu watu kuonekana wa heshima na wastaarabu kumbe walikuwa washirikina wakubwa.

Courtesy: The Global Publishers