Saturday, March 3, 2012

DAWA YA MOTO NI MOTO


Kweli uswahilini kuna vituko, hii ilitokea juzi mtaani kwetu, kuna jamaa mmoja alikuwa ni fundi wa pikipiki lakini uwezo wake haukuwa mkubwa zaidi ya kupata kipato cha kula tofauti na majirani wenzake mambo yao yalikuwa mazuri. Ilikuwa kila ikifika usiku wake zao walikuwa wakishindana kupiga muziki kwa sauti kubwa jambo lililokuwa likimkera yule msela ambaye hakuwa na redio kubwa zaidi ya redio ya simu yake ambayo ilimsaidia kusikiliza taarifa ya habari na michezo.
 
Baada ya kuvumilia sana mwisho wake uzalendo ulimshinda na kuamua kwenda kuwaeleza jirani zake.
“Jamani usiku ni wakati wa kupumzika inakuwaje tunapigiana kelele, punguzeni sauti za redio zenu.”
Majibu aliyopewa yalikuwa ya nyodo:
“Kaka acha roho ya kwa nini, kanunue yako upige tuone nani atakukataza.”
Jamaa hakujibu alijikuta akibadili muda wa kurudi nyumbani ili kujiepusha na kelele, siku moja alimweleza rafiki yake kero anayopata kwa jirani zake. Rafiki yake alimweleza dawa ya kuwakomesha aende na pikipiki isiyo na ekisozi ambayo ina mlio mbaya, usiku wenzake wakilala yeye aiwashe na kupiga lesi, kelele za pikipiki lazima zitawakera.

 
Jamaa siku ya pili alirudi nyumbani na pikipiki ya mteja isiyo na ekisozi na kuingia nayo ndani. Kama kawaida jirani zake walishindana kupiga muziki mpaka majira ya saa sita walizima na kulala, hapo ndipo msela alipowasha pikipiki na kupiga lesi iliyosababisha jirani zake wasilale kwa kelele.
Jamaa walimgongea na kumweleza anawapigia kelele naye aliwajibu:
“Na ninyi nunueni pikipiki mpige lesi muone kama nitakuja kuwazuia.”
Kauli ile iliwafanya wanyamaze kimya na tokea siku hiyo redio zilipigwa kwa sauti ya chini. Lakini jamaa ili kuwakomoa alifanya vile kwa siku tatu mfululizo na kuwafanya majirani wamuombe radhi ndipo alipoacha na heshima ikiwa mtindo mmoja.
“Hiyo ndiyo dawa ya watu kama nyinyi, nilipowaomba mpunguze sauti za redio zenu mkaleta nyodo, kweli dawa ya moto ni moto ningewalegezea mngenipanda kichwani,” jamaa huyo alijisemea akiwa chumbani kwake.


Courtesy : The GlobalPublishers